Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Samweli 20:13-26

2 Samweli 20:13-26 NEN

Baada ya Amasa kuondolewa kutoka barabarani, watu wote walienda pamoja na Yoabu kumfuatia Sheba mwana wa Bikri. Sheba akapita katika makabila yote ya Israeli hadi Abel-Beth-Maaka na kupitia eneo lote la Waberi ambao walijikusanya pamoja na kumfuata. Vikosi vyote vya Yoabu vikaja na kumhusuru Sheba mwana wa Bikri huko Abel-Beth-Maaka. Wakauzingira mji kwa kuweka vikosi vya askari, ili kukabiliana na ngome ya mji. Walipokuwa wanagongagonga ukuta ili kuubomoa na kuuangusha chini, mwanamke mmoja mwenye busara akaita kutoka ndani ya mji, akisema, “Sikilizeni! Sikilizeni! Mwambieni Yoabu aje hapa ili niweze kuzungumza naye.” Yoabu alikwenda mbele yake, akamuuliza, “Wewe ni Yoabu?” Akamjibu, “Ndiye mimi.” Yule mwanamke akamwambia, “Sikiliza kile mtumishi wako atakachokuambia.” Akamwambia, “Ninasikiliza.” Huyo mwanamke akaendelea kusema, “Zamani za kale walikuwa wakisema, ‘Wakaulize ushauri huko Abeli,’ hivyo kulimaliza lile shauri. Sisi ni watu wa amani na waaminifu katika Israeli. Wewe unajaribu kuharibu mji ambao ni mama katika Israeli. Kwa nini unataka kumeza urithi wa BWANA?” Yoabu akajibu, “Hilo liwe mbali nami. Hilo liwe mbali nami kumeza au kuharibu. Hivyo sivyo ilivyo. Mtu mmoja jina lake Sheba mwana wa Bikri, kutoka nchi ya vilima vya Efraimu, ameinua mkono wake dhidi ya mfalme, dhidi ya Daudi. Nikabidhini mtu huyu mmoja, nami nitajiondoa katika mji huu.” Huyu mwanamke akamwambia Yoabu, “Kichwa chake mtatupiwa kupitia juu ya ukuta.” Ndipo huyo mwanamke akaenda kwa watu wote akiwa na ushauri wake wa busara, nao wakakata kichwa cha Sheba mwana wa Bikri na kumtupia Yoabu. Kwa hiyo Yoabu akapiga tarumbeta, na watu wake wakatawanyika kutoka mjini, kila mmoja akirejea nyumbani kwake. Naye Yoabu akarudi kwa mfalme huko Yerusalemu. Yoabu alikuwa jemadari wa jeshi lote la Israeli; Benaya mwana wa Yehoyada alikuwa juu ya Wakerethi na Wapelethi; Adoramu alikuwa kiongozi wa wale waliofanya kazi ya kulazimishwa; Yehoshafati mwana wa Ahiludi alikuwa mweka kumbukumbu; Sheva alikuwa mwandishi; Sadoki na Abiathari walikuwa makuhani; na Ira, Myairi, alikuwa kuhani wa Daudi.