2 Samweli 2:12-32
2 Samweli 2:12-32 NEN
Abneri mwana wa Neri, pamoja na watu wa Ish-Boshethi mwana wa Sauli, wakatoka Mahanaimu kwenda Gibeoni. Yoabu mwana wa Seruya na watu wa Daudi wakatoka na kukutana nao kwenye bwawa la Gibeoni. Kikundi kimoja kiliketi upande mmoja wa bwawa, na kikundi kingine upande wa pili. Ndipo Abneri akamwambia Yoabu, “Tuwaweke baadhi ya vijana wasimame na wapigane ana kwa ana mbele yetu.” Yoabu akasema, “Sawa, na wafanye hivyo.” Kwa hiyo vijana wakasimama, wakahesabiwa: watu wa Benyamini na wa Ish-Boshethi mwana wa Sauli kumi na wawili, na upande wa Daudi kumi na wawili. Kisha kila mtu akakamatana na mpinzani wake kichwani na kuchomana kwa upanga, nao wakaanguka chini pamoja. Kwa hiyo mahali pale katika Gibeoni pakaitwa Helkath-Hasurimu. Siku hiyo vita vilikuwa vikali sana, naye Abneri na watu wa Israeli wakashindwa na watu wa Daudi. Wana watatu wa Seruya walikuwako huko: nao ni Yoabu, Abishai na Asaheli. Basi huyo Asaheli alikuwa na mbio kama paa. Asaheli akamfukuza Abneri, pasipo kugeuka kulia wala kushoto wakati akimfuata. Abneri akaangalia nyuma na kumuuliza, “Ni wewe, Asaheli?” Akamjibu, “Ndiyo.” Ndipo Abneri akamwambia, “Geuka upande wa kulia au kushoto. Mchukue mmoja wa vijana wa kiume na umvue silaha zake.” Lakini Asaheli hakuacha kumfukuza. Abneri akamwonya tena Asaheli akimwambia, “Acha kunifukuza! Kwa nini nikuue? Je, nitawezaje kumtazama ndugu yako Yoabu usoni?” Lakini Asaheli alikataa kuacha kumfuatia, kwa hiyo Abneri akamchoma Asaheli tumboni kwa ncha butu ya mkuki wake, mkuki ukamtoboa ukatokea mgongoni mwake. Akaanguka na kufa papo hapo. Ikawa kila mtu alisimama alipofika mahali pale Asaheli alipoanguka na kufa. Lakini Yoabu na Abishai walimfuata Abneri, na jua lilipokuwa linatua, wakafika kwenye kilima cha Ama, karibu na Gia kwenye njia ya kuelekea kwenye nyika ya Gibeoni. Ndipo watu wa kabila la Benyamini wakakusanyika tena nyuma ya Abneri. Wakaunda kikosi na kujiimarisha juu ya kilima. Abneri akamwita Yoabu, akamwambia, “Je, ni lazima upanga uendelee kuangamiza milele? Hutambui kwamba jambo hili litaishia katika uchungu? Utaacha kuwaagiza watu wako waache kuwafuatilia ndugu zao hata lini?” Yoabu akajibu, “Hakika kama aishivyo Mungu, kama hukusema, hawa watu wangeendelea kuwafuatia ndugu zao mpaka asubuhi.” Basi Yoabu akapiga tarumbeta, nao watu wote wakasimama, hawakuwafuata Israeli tena, wala hawakuwapiga tena. Usiku ule wote Abneri na watu wake wakatembea kupitia Araba. Wakavuka Mto Yordani, wakaendelea wakipitia nchi yote ya Bithroni wakafika Mahanaimu. Basi Yoabu akarudi kutoka kumfuatia Abneri, na kuwakusanya watu wake wote. Pamoja na Asaheli, watu kumi na tisa wa Daudi walikuwa wamepotea. Lakini watu wa Daudi walikuwa wamewaua watu wa kabila la Benyamini 360 waliokuwa pamoja na Abneri. Wakamchukua Asaheli, wakamzika katika kaburi la baba yake huko Bethlehemu. Kisha Yoabu na watu wake wakatembea usiku kucha na kufika huko Hebroni wakati wa mapambazuko.