2 Samweli 16:15-23
2 Samweli 16:15-23 NENO
Wakati huo, Absalomu pamoja na wanaume wote wa Israeli wakafika Yerusalemu, naye Ahithofeli alikuwa pamoja naye. Ndipo Hushai Mwarki, rafiki wa Daudi, akamwendea Absalomu na kumwambia, “Mfalme aishi maisha marefu! Mfalme aishi maisha marefu!” Absalomu akamuuliza Hushai, “Je, huu ndio upendo unaomwonesha rafiki yako? Kwa nini hukufuatana na rafiki yako?” Hushai akamwambia Absalomu, “La hasha! Yeye aliyechaguliwa na Mwenyezi Mungu, aliyechaguliwa na watu hawa, atakayechaguliwa tena na wanaume wote wa Israeli, huyu ndiye nitakayekuwa wake, nami nitabakia pamoja naye. Zaidi ya hayo, nimtumikie nani? Je, nisimtumikie mwana? Kama vile nilivyomtumikia baba yako, ndivyo nitakavyokutumikia wewe.” Absalomu akamwambia Ahithofeli, “Tupe ushauri wako. Tufanye nini?” Ahithofeli akamjibu Absalomu, “Kutana kimwili na masuria wa baba yako aliowaacha kutunza jumba la kifalme. Ndipo Israeli yote itakaposikia kwamba umejifanya chukizo kwa baba yako, nayo mikono ya kila mmoja aliye pamoja nawe itatiwa nguvu.” Kwa hiyo wakamtengenezea Absalomu hema juu ya dari, naye akakutana kimwili na masuria wa baba yake machoni pa Israeli wote. Ilikuwa katika siku hizo shauri lililotolewa na Ahithofeli lilikuwa kama lile ambalo limeulizwa kwa Mungu. Ndivyo Daudi na Absalomu walivyoyaheshimu mashauri yote ya Ahithofeli.