Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

2 Samweli 10:1-19

2 Samweli 10:1-19 NENO

Baada ya muda, mfalme wa Waamoni akafa, naye Hanuni mwanawe akawa mfalme baada yake. Daudi akawaza, “Nitamtendea wema Hanuni mwana wa Nahashi, kama vile baba yake alivyonitendea mimi wema.” Hivyo Daudi akatuma wajumbe kuonesha wema wake kwa Hanuni kuhusu baba yake. Watu wa Daudi walipofika katika nchi ya Waamoni, wakuu wa Waamoni wakamwambia Hanuni bwana wao, “Unadhani Daudi anamheshimu baba yako kwa kukutumia watu ili kuonesha masikitiko? Je, Daudi hakuwatuma watu hawa kuchunguza na kuupeleleza mji ili kuupindua?” Basi Hanuni akawakamata watu wa Daudi, akawanyoa kila mmoja ndevu zake nusu, akakata mavazi yao nyuma katikati kwenye matako, akawaachia waende zao. Daudi alipoambiwa jambo hili, akatuma wajumbe ili kwenda kuwalaki, kwa maana walikuwa wamevunjiwa heshima sana. Mfalme akasema, “Kaeni huko Yeriko hadi ndevu zenu ziote, ndipo mje.” Waamoni walipotambua kuwa wamekuwa machukizo kwa Daudi, wakaajiri askari wa miguu elfu ishirini, Waaramu kutoka Beth-Rehobu na Soba, pia mfalme wa Maaka na watu elfu moja, na vilevile watu elfu kumi na mbili kutoka Tobu. Daudi aliposikia jambo hili, akamtuma Yoabu na jeshi lote la wapiganaji. Waamoni wakatoka wakajipanga wakiwa tayari kwa vita langoni la mji wao, wakati Waaramu wa Soba na wa Rehobu, na wanaume wa Tobu na Maaka walikuwa peke yao kwenye eneo la wazi. Yoabu akaona kuwa mbele yake na nyuma yake kumepangwa vita; kwa hiyo akachagua baadhi ya vikosi vilivyo bora sana katika Israeli akavipanga dhidi ya Waaramu. Akawaweka waliobaki chini ya uongozi wa Abishai nduguye na kuwapanga dhidi ya Waamoni. Yoabu akasema, “Kama Waaramu watanizidi nguvu, basi itawabidi mje kunisaidia. Lakini kama Waamoni watawazidi nguvu, basi nitakuja kuwasaidia. Uwe hodari na tupigane kwa ujasiri kwa ajili ya watu wetu na miji ya Mungu wetu. Mwenyezi Mungu atafanya lile lililo jema machoni pake.” Basi Yoabu na vikosi vyake wakasonga mbele kupigana na Waaramu, nao Waaramu wakakimbia mbele yake. Waamoni walipoona Waaramu wanakimbia, nao wakakimbia mbele ya Abishai na kuingia ndani ya mji. Basi Yoabu akarudi kutoka kupigana na Waamoni na kufika Yerusalemu. Baada ya Waaramu kuona wameshindwa na Israeli, wakajikusanya tena. Hadadezeri akaagiza Waaramu walioletwa kutoka ng’ambo ya Mto, wakaenda Helamu pamoja na Shobaki jemadari wa jeshi la Hadadezeri akiwaongoza. Daudi alipoambiwa haya, akawakusanya Israeli wote, wakavuka Mto Yordani, wakaenda Helamu. Waaramu wakapanga vikosi vyao vya askari kukabiliana na kupigana dhidi ya Daudi. Lakini Waaramu wakakimbia mbele ya Israeli, naye Daudi akawaua waendesha magari ya vita mia saba na askari wao wa miguu elfu arobaini. Vilevile alimpiga Shobaki jemadari wa jeshi lao, naye akafa huko. Wafalme wote waliokuwa wanamtumikia Hadadezeri walipoona kuwa wameshindwa na Israeli, wakafanya amani na Waisraeli na wakawa chini yao. Hivyo Waaramu wakaogopa kuwasaidia Waamoni tena.