1 Timotheo 6:11-20
1 Timotheo 6:11-20 NENO
Lakini wewe, mtu wa Mungu, yakimbie mambo haya yote. Fuata haki, utauwa, imani, upendo, saburi na upole. Pigana vile vita vizuri vya imani. Shika uzima wa milele ambao ndio ulioitiwa ulipokiri ule ukiri mzuri mbele ya mashahidi wengi. Nakuagiza mbele za Mungu avipaye vitu vyote uhai, na mbele za Kristo Yesu, ambaye alipokuwa anashuhudia mbele ya Pontio Pilato alikiri ukiri mzuri, uishike amri hii bila dosari wala lawama hadi kufunuliwa kwake Bwana wetu Yesu Kristo; ambako Mungu atadhihirisha kwa wakati wake mwenyewe: Mungu ahimidiwaye, aliye peke yake Mtawala, Mfalme wa wafalme, na Bwana wa mabwana, yeye pekee aishiye milele, anayedumu katika nuru isiyoweza kukaribiwa, ambaye hakuna mwanadamu aliyemwona wala awezaye kumwona. Heshima na uweza una yeye milele. Amen. Waagize wale ambao ni matajiri wa ulimwengu huu waache kujivuna, wala wasiweke tumaini lao katika mali ambayo si ya hakika, bali waweke tumaini lao katika Mungu ambaye hutupatia vitu vyote kwa wingi ili tuvifurahie. Waagize watende mema, wawe matajiri katika matendo mema, pia wawe wakarimu na walio tayari kushiriki mali yao na wengine. Kwa njia hii watajiwekea hazina kama msingi kwa ajili ya wakati ujao na hivyo watajipatia uzima, yaani ule uzima ambao ni wa kweli. Timotheo, linda kile kilichowekwa amana kwako. Epuka majadiliano yasiyo ya utauwa na mabishano ambayo kwa uongo huitwa elimu