1 Samweli 28:1-14
1 Samweli 28:1-14 NENO
Siku zile Wafilisti wakakusanya majeshi yao ili kupigana vita dhidi ya Israeli. Akishi akamwambia Daudi, “Lazima ujue kuwa wewe pamoja na watu wako mtafuatana nami kwenda vitani.” Daudi akasema, “Ndipo wewe mwenyewe utakapojionea jambo ambalo mtumishi wako anaweza kufanya.” Akishi akamjibu Daudi, “Vyema sana, mimi nitakufanya uwe mlinzi wangu daima.” Wakati huo Samweli alikuwa amekufa, nao Waisraeli wote walikuwa wamemwombolezea na kumzika kwenye mji wake mwenyewe huko Rama. Sauli alikuwa amewafukuza waaguzi na wachawi. Wafilisti wakakusanyika na kupiga kambi yao huko Shunemu, naye Sauli akawakusanya Waisraeli wote na kupiga kambi yao huko Gilboa. Sauli alipoona jeshi la Wafilisti, akaogopa; moyo wake ukajawa na hofu kuu. Ndipo Sauli akauliza ushauri kwa BWANA, lakini BWANA hakumjibu kwa ndoto, wala kwa Urimu, wala kupitia manabii. Basi Sauli akawaambia watumishi wake, “Nitafutieni mwanamke mwaguzi ili nimwendee, nipate kuuliza kwake.” Watumishi wake wakamwambia, “Yuko mwanamke mmoja huko Endori.” Hivyo Sauli akajigeuza kwa kuvaa mavazi mengine, naye usiku akiwa amefuatana na watu wawili wakaenda kwa huyo mwanamke. Akamwambia, “Nibashirie kwa uaguzi, unipandishie yule nitakayekutajia.” Huyo mwanamke akamwambia, “Wewe unajua lile alilofanya Mfalme Sauli. Amewakatilia mbali waaguzi, wapiga ramli wote na wachawi katika nchi. Mbona umenitegea maisha yangu ili wapate kuniua?” Sauli akamwapia huyo mwanamke kwa Jina la BWANA, akasema, “Kwa hakika kama BWANA aishivyo, hutaadhibiwa kwa ajili ya jambo hili.” Ndipo yule mwanamke akauliza, “Je unataka nikupandishie nani?” Sauli akasema, “Nipandishie Samweli.” Yule mwanamke alipomwona Samweli, alipiga yowe kwa sauti kuu, naye akamuuliza Sauli, “Mbona umenidanganya? Wewe ndiwe Sauli.” Mfalme akamwambia, “Usiogope. Unaona nini?” Yule mwanamke akasema, “Naona mungu unapanda kutoka ardhini.” Sauli akamuuliza, “Ni mfano wa nini?” Yule mwanamke akasema, “Ni mwanaume mzee amevaa joho anayepanda.” Ndipo Sauli akatambua kwamba ni Samweli. Sauli akasujudu, uso wake ukagusa chini.