1 Samweli 17:1-19
1 Samweli 17:1-19 NENO
Wakati huo Wafilisti wakakusanya majeshi yao kwa ajili ya vita, nao wakakusanyika huko Soko katika Yuda. Wakapiga kambi huko Efes-Damimu, kati ya Soko na Azeka. Sauli na Waisraeli wakakusanyika na kupiga kambi katika Bonde la Ela na kupanga jeshi ili kupigana vita na Wafilisti. Wafilisti wakawa katika kilima kimoja, na Waisraeli katika kilima kingine, nalo bonde likiwa kati yao. Shujaa aliyeitwa Goliathi, aliyetoka Gathi, akajitokeza kutoka kambi ya Wafilisti. Alikuwa na urefu dhiraa sita na shibiri moja. Alikuwa na chapeo ya shaba kichwani mwake, na alivaa dirii ya shaba kifuani mwake yenye uzito wa shekeli elfu tano. Miguuni mwake alivaa mabamba ya shaba, na alikuwa na mkuki wa shaba mgongoni mwake. Mpini wa huo mkuki ulikuwa kama mti wa mfumaji, na ncha ya chuma yake ilikuwa na uzito wa shekeli mia sita. Mbeba ngao wake alitangulia mbele yake. Goliathi alisimama na kuwaambia majeshi ya Israeli kwa sauti kuu, akisema, “Kwa nini mmetoka kupanga vita? Je, mimi si Mfilisti, na ninyi ni watumishi wa Sauli? Chagueni mtu na anishukie mimi. Kama anaweza kupigana nami na kuniua, tutakuwa chini yenu; lakini nikimshinda na kumuua, ninyi mtakuwa chini yetu, na mtatutumikia.” Kisha yule Mfilisti akasema, “Siku hii ya leo nayatukana majeshi ya Israeli! Nipeni mtu tupigane.” Kwa kusikia maneno ya Wafilisti, Sauli na Waisraeli wote wakafadhaika na kuogopa. Basi Daudi alikuwa mwana wa Mwefrathi jina lake Yese aliyekuwa ametoka Bethlehemu ya Yuda. Yese alikuwa na wana wanane, naye wakati wa Sauli alikuwa mzee sana. Wana wakubwa watatu wa Yese walikuwa wamefuatana na Sauli vitani: Mzaliwa wa kwanza alikuwa Eliabu, wa pili Abinadabu, na wa tatu Shama. Daudi ndiye alikuwa mdogo wa wote. Hao wakubwa watatu wakamfuata Sauli, lakini Daudi alikuwa akienda kwa Sauli na kurudi ili kuchunga kondoo wa baba yake huko Bethlehemu. Kwa siku arobaini huyo Mfilisti alikuwa akija mbele kila siku asubuhi na jioni na kujionesha. Wakati huo Yese akamwambia mwanawe Daudi, “Chukua hii efa ya bisi na hii mikate kumi kwa ajili ya ndugu zako uwapelekee upesi kambini mwao. Chukua pamoja na hizi jibini kumi kwa jemadari wa kikosi chao. Ujue hali ya ndugu zako na uniletee taarifa za uhakika kutoka kwao. Wao wako pamoja na Sauli na wanaume wote wa Israeli huko kwenye Bonde la Ela, wakipigana na Wafilisti.”