1 Wafalme 8:41-53
1 Wafalme 8:41-53 NEN
“Kwa habari ya mgeni ambaye si miongoni mwa watu wako Israeli, lakini amekuja kutoka nchi ya mbali kwa sababu ya jina lako, kwa maana watu watasikia juu ya Jina lako kuu na juu ya mkono wako wenye nguvu na mkono wako ulionyooshwa, atakapokuja na kuomba kuelekea Hekalu hili, basi na usikie kutoka mbinguni, mahali pa makao yako, ukafanye lolote ambalo mgeni huyo anakuomba, ili mataifa yote ya dunia wapate kujua jina lako na wakuogope kama wafanyavyo watu wako Israeli nao wapate pia kujua kwamba nyumba hii niliyoijenga imeitwa kwa Jina lako. “Wakati watu wako watakapokwenda vitani dhidi ya adui zao, popote utakapowapeleka, wakati watakapoomba kwa BWANA kuelekea mji ambao umeuchagua, na Hekalu nililolijenga kwa ajili ya Jina lako, basi usikie dua na maombi yao kutoka mbinguni, ukawatetee haki yao. “Watakapotenda dhambi dhidi yako, kwa kuwa hakuna mtu yeyote ambaye hatendi dhambi, nawe ukachukizwa nao na kuwakabidhi kwa adui, ambaye atawachukua utumwani katika nchi yake mwenyewe, mbali au karibu; na kama watabadilika mioyo yao katika nchi wanakoshikiliwa mateka, nao wakatubu na kukulilia katika nchi ya wale waliowashinda na kusema, ‘Tumetenda dhambi, tumefanya makosa, tumetenda uovu’; kama wakikugeukia kwa moyo wao wote na nafsi zao katika nchi ya adui zao ambao waliwachukua mateka, wakakuomba kuelekea nchi uliyowapa baba zao, kuelekea mji uliouchagua na Hekalu nililolijenga kwa ajili ya Jina lako; basi kutoka mbinguni, mahali pa makao yako, usikie dua yao na maombi yao na kuitetea haki yao. Uwasamehe watu wako, waliotenda dhambi dhidi yako; uwasamehe makosa yote waliyoyatenda dhidi yako, ukawafanye wale waliowashinda kuwaonea huruma; kwa maana ni watu wako na urithi wako, uliowatoa Misri, kutoka kwenye lile tanuru la kuyeyushia chuma. “Macho yako na yafumbuke juu ya ombi la mtumishi wako na ombi la watu wako Israeli, nawe uwasikilize wakati wowote wanapokulilia. Kwa maana uliwachagua wao kutoka mataifa yote ya ulimwengu kuwa urithi wako mwenyewe, kama ulivyotangaza kupitia mtumishi wako Mose wakati wewe, Ee BWANA Mwenyezi, ulipowatoa baba zetu kutoka Misri.”