Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 18:22-38

1 Wafalme 18:22-38 NEN

Kisha Eliya akawaambia, “Ni mimi peke yangu nabii wa BWANA aliyebaki, lakini Baali ana manabii mia nne na hamsini. Leteni mafahali wawili. Wao na wajichagulie mmoja, wamkate vipande vipande na waweke juu ya kuni lakini wasiiwashie moto. Nitamwandaa huyo fahali mwingine na kumweka juu ya kuni lakini sitawasha moto. Kisha mliitie jina la mungu wenu, nami nitaliitia jina la BWANA Mungu yule ambaye atajibu kwa moto, huyo ndiye Mungu.” Kisha watu wote wakasema, “Hilo unalosema ni jema.” Eliya akawaambia manabii wa Baali, “Chagueni mmoja kati ya hawa mafahali na mwe wa kwanza kumwandaa, kwa kuwa ninyi mko wengi sana. Liitieni jina la mungu wenu, lakini msiwashe moto.” Kwa hiyo wakamchukua yule fahali waliyepewa, nao wakamwandaa. Kisha wakaliitia jina la Baali kutoka asubuhi hadi adhuhuri, wakapiga kelele, “Ee Baali, utujibu!” Lakini hapakuwa na jibu; hakuna aliyejibu. Nao wakacheza kuizunguka madhabahu waliyoijenga. Wakati wa adhuhuri, Eliya akaanza kuwadhihaki, akisema, “Pigeni kelele zaidi! Hakika yeye ni mungu! Labda amezama katika mawazo mazito, au ana shughuli nyingi, au amesafiri. Labda amelala usingizi mzito, naye ni lazima aamshwe.” Kwa hiyo wakapiga kelele zaidi na kama ilivyokuwa desturi yao wakajichanja wenyewe kwa visu na vyembe, mpaka damu ikachuruzika. Adhuhuri ikapita, nao wakaendelea na utabiri wao wa kiwazimu mpaka wakati wa dhabihu ya jioni. Lakini hapakuwa na jibu, hakuna aliyejibu, hakuna aliyeangalia. Kisha Eliya akawaambia watu wote, “Sogeeni karibu nami.” Watu wote wakamkaribia, naye akakarabati madhabahu ya BWANA, ambayo ilikuwa imevunjwa. Eliya akachukua mawe kumi na mawili, moja kwa ajili ya kila kabila la wana wa Yakobo, ambaye neno la BWANA lilimjia, likisema, “Jina lako litakuwa Israeli.” Kwa mawe hayo, akajenga madhabahu katika jina la BWANA, na akachimba handaki kuizunguka, ukubwa wa kutosha vipimo viwili vya mbegu. Akapanga kuni, akamkata yule fahali vipande vipande na kuvipanga juu ya kuni. Kisha akawaambia, “Jazeni mapipa manne maji na kuyamwaga juu ya sadaka ya kuteketezwa na juu ya kuni.” Akawaambia, “Fanyeni hivyo tena.” Nao wakafanya hivyo tena. Akaagiza, “Fanyeni kwa mara ya tatu.” Nao wakafanya hivyo kwa mara ya tatu. Maji yakatiririka kuizunguka madhabahu na hata kujaza lile handaki. Wakati wa kutoa dhabihu ya jioni, nabii Eliya akasogea mbele na kuomba, akisema: “Ee BWANA, Mungu wa Abrahamu, na Isaki na Israeli, ijulikane leo kwamba wewe ndiye Mungu katika Israeli na ya kwamba mimi ni mtumishi wako na nimefanya mambo haya yote kwa neno lako. Unijibu mimi, Ee BWANA, nijibu mimi, ili watu hawa wajue kwamba wewe, Ee BWANA, ndiwe Mungu, na kwamba unaigeuza mioyo yao ikurudie tena.” Kisha moto wa BWANA ukashuka na kuiteketeza ile dhabihu, zile kuni, yale mawe, ule udongo, na pia kuramba yale maji yaliyokuwa ndani ya handaki.

YouVersion hutumia vidakuzi kubinafsisha matumizi yako. Kwa kutumia tovuti yetu, unakubali matumizi yetu ya vidakuzi kama ilivyoelezwa katika Sera yetu ya Faragha