Chapa ya Youversion
Ikoni ya Utafutaji

1 Wafalme 1:11-21

1 Wafalme 1:11-21 NEN

Ndipo Nathani akamuuliza Bathsheba, mama yake Solomoni, “Je, hujasikia kwamba Adoniya, mwana wa Hagithi, amekuwa mfalme pasipo bwana wetu Daudi kujua jambo hili? Sasa basi, acha nikushauri jinsi utakavyookoa uhai wako mwenyewe na uhai wa mwanao Solomoni. Ingia kwa Mfalme Daudi na umwambie, ‘Bwana wangu mfalme, je hukuniapia mimi mtumishi wako: “Hakika mwanao Solomoni atakuwa mfalme baada yangu na ndiye atakayeketi juu ya kiti changu cha ufalme”? Kwa nini basi Adoniya amekuwa mfalme?’ Utakapokuwa ukizungumza na mfalme, nitaingia na kuthibitisha hayo uliyoyasema.” Hivyo Bathsheba akaenda kumwona mfalme chumbani mwake mahali ambapo Abishagi, Mshunami, alikuwa akimhudumia, naye mfalme alikuwa mzee sana. Bathsheba akasujudu na kupiga magoti mbele ya mfalme. Mfalme akauliza, “Ni nini hiki unachotaka?” Akamwambia, “Bwana wangu, wewe mwenyewe uliniapia mimi mtumishi wako kwa BWANA Mungu wako kwamba: ‘Solomoni Mwanao atakuwa mfalme baada yangu na ndiye atakayeketi kwenye kiti changu cha ufalme.’ Lakini sasa Adoniya amekuwa mfalme, nawe, bwana wangu mfalme huna habari kuhusu jambo hilo. Ametoa dhabihu idadi kubwa ya ngʼombe, ndama walionona na kondoo, naye amewaalika wana wa mfalme wote, kuhani Abiathari, na Yoabu jemadari wa jeshi, lakini hakumwalika Solomoni mtumishi wako. Bwana wangu mfalme, macho ya Israeli yote yanakutazama wewe wajue kutoka kwako kuwa ni nani atakayeketi katika kiti cha ufalme cha bwana wangu mfalme baada yake. Kama sivyo, mara tu bwana wangu mfalme atakapopumzishwa pamoja na baba zake, mimi na mwanangu Solomoni tutatendewa kama wahalifu.”