1 Wakorintho 6:1-8
1 Wakorintho 6:1-8 NENO
Kama mtu yeyote wa kwenu ana ugomvi na mwenzake, anathubutuje kuupeleka kwa wasiomcha Mungu ili kuamuliwa badala ya kuupeleka kwa watakatifu? Je, hamjui kwamba watakatifu watauhukumu ulimwengu? Nanyi kama mtauhukumu ulimwengu, je, hamwezi kuamua mambo madogo madogo? Hamjui kwamba tutawahukumu malaika? Je, si zaidi mambo ya maisha haya? Kwa hiyo kama kuna ugomvi miongoni mwenu kuhusu mambo kama haya, je, mnachagua watu ambao wanaonekana hata sio wa heshima katika kundi la waumini kuwa waamuzi kati yenu? Nasema hivi ili mwone aibu. Je, inawezekana kuwa miongoni mwenu hakuna mtu mwenye hekima ya kutosha kuamua ugomvi kati ya waumini? Badala yake ndugu mmoja anampeleka mwenzake mahakamani, tena mbele ya watu wasioamini! Huko kuwa na mashtaka miongoni mwenu ina maana kwamba tayari ni kushindwa kabisa. Kwa nini msikubali kutendewa mabaya? Kwa nini msikubali kunyang’anywa? Badala yake, ninyi wenyewe mwadanganya na kutenda mabaya, tena mwawatendea ndugu zenu.