1 Wakorintho 5:6-13
1 Wakorintho 5:6-13 NENO
Majivuno yenu si mazuri. Je, hamjui kwamba chachu kidogo huchachusha donge zima la unga? Ondoeni chachu ya kale ili mpate kuwa donge jipya lisilotiwa chachu, kama vile mlivyo. Kwa maana Al-Masihi, Mwana-Kondoo wetu wa Pasaka amekwisha tolewa kuwa dhabihu. Kwa hiyo, tusiiadhimishe sikukuu hii kwa chachu ya zamani, chachu ya nia mbaya na uovu, bali kwa mkate usiotiwa chachu, ndio weupe wa moyo na kweli. Niliwaandikia katika waraka wangu kuwa msishirikiane na wazinzi. Sina maana kwamba msishirikiane na wazinzi wa ulimwengu huu, au wenye tamaa mbaya, wanyang’anyi au waabudu sanamu. Kwa kufanya hivyo ingewalazimu mtoke ulimwenguni humu. Lakini sasa nawaandikia kwamba msishirikiane na mtu yeyote anayejiita ndugu, hali akiwa ni mzinzi, au mwenye tamaa mbaya, mwabudu sanamu au msingiziaji, mlevi au mdhalimu. Mtu kama huyo hata msile naye. Yanihusu nini kuwahukumu wale watu walio nje ya kundi la waumini? Je, si mnapaswa kuwahukumu hao walio ndani? Mungu atawahukumu hao walio nje. “Ninyi mwondoeni huyo mtu mwovu miongoni mwenu.”