1 Wakorintho 12:1-8
1 Wakorintho 12:1-8 NEN
Basi ndugu zangu, kuhusu karama za rohoni, sitaki mkose kufahamu. Mnajua kwamba mlipokuwa watu wasiomjua Mungu, kwa njia moja au ingine mlishawishika na kupotoshwa mkielekezwa kwa sanamu zisizonena. Kwa hiyo nawaambieni ya kuwa hakuna mtu anayeongozwa na Roho wa Mungu anayeweza kusema, “Yesu na alaaniwe.” Pia hakuna mtu awezaye kusema, “Yesu ni Bwana,” isipokuwa ameongozwa na Roho Mtakatifu. Kuna aina mbalimbali za karama, lakini Roho ni yule yule. Kuna huduma za aina mbalimbali, lakini Bwana ni yule yule. Kisha kuna tofauti za kutenda kazi, lakini ni Mungu yule yule atendaye kazi zote kwa watu wote. Basi kila mmoja hupewa ufunuo wa Roho kwa faida ya wote. Maana mtu mmoja kwa Roho hupewa neno la hekima na mwingine neno la maarifa kwa Roho huyo huyo.