Mathayo 11
11
Yohana Atuma Watu Kumwuliza Yesu Swali
(Lk 7:18-35)
1Yesu alipomaliza maelekezo haya kwa wafuasi wake kumi na wawili wa karibu, aliondoka mahali pale. Akaenda katika miji ya Galilaya kuwafundisha watu na kuwaeleza ujumbe wa Mungu.
2Yohana alipokuwa gerezani, alisikia kuhusu mambo yaliyokuwa yanatokea; mambo ambayo Masihi angefanya. Hivyo akawatuma baadhi ya wafuasi wake kwa Yesu. 3Wakamuuliza, “Wewe ni yule tuliyekuwa tunamngojea, au tumsubiri mwingine?”
4Yesu akajibu, “Rudini mkamwambie Yohana yale mliyosikia na kuona: 5Vipofu wanaona. Viwete wanatembea. Watu wenye magonjwa ya ngozi wanaponywa. Wasiyesikia wanasikia. Wafu wanafufuliwa. Na habari njema inahubiriwa kwa maskini. 6Heri ni kwa wale wasio na shida kunikubali.”
7Wafuasi wa Yohana walipoondoka, Yesu alianza kuongea na watu kuhusu Yohana. Alisema, “Ninyi watu mlikwenda jangwani kuona nini? Mtu aliye dhaifu, kama unyasi unaoyumbishwa na upepo? 8Hakika, ni nini mlichotarajia kuona? Aliyevaa mavazi mazuri? Hakika si hivyo. Watu wote wanaovaa mavazi mazuri wanapatikana katika ikulu za wafalme. 9Hivyo mlitoka kuona nini? Nabii? Ndiyo, Yohana ni nabii. Lakini ninawaambia, Yeye ni zaidi ya hilo. 10Andiko hili liliandikwa kuhusu Yohana:
‘Sikiliza! Nitamtuma mjumbe mbele yako.
Yeye ataandaa njia kwa ajili yako.’#Mal 3:1
11Ukweli ni kuwa Yohana Mbatizaji ni mkuu kuliko yeyote aliyewahi kuja katika ulimwengu huu. Lakini hata mtu asiye wa muhimu katika ufalme wa Mungu ni mkuu kuliko Yohana. 12Tangu wakati wa Yohana Mbatizaji ulipokuja mpaka sasa, Ufalme wa Mungu umekabiliwa na mashambulizi. Watu wenye nguvu wamejaribu kuudhibiti ufalme huu.#11:12 Herode Antipa alimkamata na kisha kumwua Yohana Mbatizaji na pia alijaribu kumzuia Yesu na wanafunzi wake kwa nguvu. Tazama Herode katika Orodha ya Maneno. 13Kabla ya Yohana kuja, Sheria ya Musa na manabii wote wamesema kuhusu mambo ambayo yangetokea. 14Na ikiwa mnaamini waliyosema, basi Yohana ni Eliya. Ndiye waliyesema angekuja. 15Ninyi watu mnaonisikia, sikilizeni!
16Ninaweza kusema nini kuhusu watu wanaoishi leo? Watu siku ya leo ni kama watoto wanaokaa katika masoko. Kundi moja la watoto linaliambia kundi lingine,
17‘Tuliwapigia filimbi,
lakini hamkucheza;
tuliimba wimbo wa maziko,
lakini hamkuhuzunika.’
18Kwa nini ninasema watu wako hivyo? Kwa sababu Yohana alikuja na hakula vyakula vya kawaida na kunywa divai, na watu walisema, ‘Ana pepo ndani yake.’ 19Mwana wa Adamu amekuja akila na kunywa, na watu husema, ‘Mwangalie! Hula sana na kunywa divai nyingi. Ni rafiki wa wakusanya kodi na wenye dhambi wengine.’ Lakini hekima inaonesha kuwa sahihi kutokana na yale inayotenda.”
Maonyo Kwa Wanaomkataa Yesu
(Lk 10:13-15)
20Kisha Yesu akaanza kuikosoa miji ambako alifanya miujiza yake mingi. Aliikosoa miji hii kwa sababu watu katika miji hii hawakubadili maisha yao na kuacha kutenda dhambi. 21Yesu alisema, “Itakuwa vibaya kwako Korazini! Itakuwa vibaya kwako Bethsaida!#11:21 Korazini, Bethsaida Miji ya Kiyahudi iliyokuwa kando mwa Ziwa Galilaya ambapo Yesu alifanya miujiza mingi kudhihirisha mamlaka yake yanayotoka kwa Mungu. Pamoja na hili, watu walikataa kubadili maisha waliyoishi yasiyokuwa na Mungu. Ikiwa miujiza hii hii ingetokea Tiro na Sidoni,#11:21 Tiro na Sidoni Miji iliyojaa ibada ya sanamu ambayo ilijulikana sana kwa uovu uliokuwemo humo. watu huko wangeshabadili maisha yao kitambo. Wangekwishavaa magunia na kujimwagia majivu kuonesha kuwa wanasikitikia dhambi zao. 22Lakini ninawaambia, siku ya hukumu itakuwa vibaya zaidi kwako kuliko Tiro na Sidoni.
23Nawe Kapernaumu, utakwezwa mpaka mbinguni? Hapana! Utatupwa chini mpaka Kuzimu. Nimetenda miujiza mingi ndani yako. Iwapo miujiza hii ingetokea Sodoma,#11:23 Sodoma Mji ambao Mungu aliuangamiza, pamoja na Jiji la Gomora, kwa sababu watu walioishi walikuwa waovu sana. Tazama Mwa 19. watu huko wangeacha kutenda dhambi na ungekuwa bado ni mji hata leo. 24Lakini ninakuambia, itakuwa vibaya kwako siku ya hukumu kuliko Sodoma.”
Yesu Awapa Pumziko Watu Wake
(Lk 10:21-22)
25Kisha Yesu akasema, “Ninakusifu wewe, Baba, Bwana wa mbinguni na duniani. Ninashukuru kwa sababu umeyaficha mambo haya kwa wale wanaofikiri kuwa ni wenye hekima na werevu sana. Lakini umeyaonesha haya kwa watu walio kama watoto wadogo.#11:25 kama watoto wadogo Maana wale ambao hawajaenda shule bado. 26Ndiyo, Baba, ulifanya hivi kwa sababu hakika ndivyo ulivyotaka kufanya.
27Baba yangu amenipa kila kitu. Hakuna amjuaye Mwana isipokuwa Baba peke yake. Na hakuna amjuaye Baba isipokuwa Mwana ndiye anayemjua Baba. Na watu pekee watakaomjua Baba ni wale ambao Mwana atachagua kuwaonesha.
28Njooni kwangu ninyi nyote mliochoka kutokana na mizigo mizito mnayolazimishwa kubeba. Nitawapa pumziko. 29Chukueni nira yangu,#11:29 nira yangu Nira iliwekwa shingoni mwa mnyama anayefanya kazi ili kuvuta mzigo. Ilikuwa pia ni alama ya Kiyahudi kwa sheria. Tazama Mdo 15:10; Gal 5:1. Ilikuwa pia alama ya kutawaliwa na taifa katili la kigeni, kama vile Ufalme wa Rumi. jifunzeni kutoka kwangu. Mimi ni mwema na mnyenyekevu katika roho. Nanyi mtaweza kupumzika. 30Ndiyo, nira yangu ni rahisi. Mzigo ninaowapa muubebe ni mwepesi.”
Agano Jipya: Tafsiri ya Kusoma-Kwa-Urahisi
Toleo la Awali
© 2017 Bible League International