Mwanzo 17
17
Agano la Tohara
1Abramu alipokuwa na umri wa miaka tisini na tisa, Mwenyezi Mungu akamtokea, akamwambia, “Mimi ndimi Mungu Mwenyezi#17:1 Kiebrania El-Shaddai (yaani Mungu Mwenye utoshelevu wote).; nenda mbele zangu na uishi kwa unyofu. 2Nitafanya agano kati yangu na wewe, nami nitakuzidisha sana.”
3Abramu akaanguka kifudifudi, naye Mungu akamwambia, 4“Kwangu mimi, hili ndilo agano langu na wewe: Wewe utakuwa baba wa mataifa mengi. 5Hutaitwa tena Abramu#17:5 maana yake Baba aliyetukuka, bali jina lako litakuwa Ibrahimu#17:5 maana yake Baba wa wengi, kwa maana nimekufanya baba wa mataifa mengi. 6Nitakufanya uwe na uzao mwingi sana; kwako yatatoka mataifa, na wafalme watatoka kwako. 7Nitalithibitisha agano langu kama agano la milele kati yangu na wewe na wazao wako baada yako na vizazi vijavyo, nami nitakuwa Mungu wako na Mungu wa wazao wako. 8Nchi yote ya Kanaani, unayoishi sasa kama mgeni, nitakupa kuwa milki yako milele, na ya uzao wako; nami nitakuwa Mungu wao.”
9Ndipo Mungu akamwambia Ibrahimu, “Kwako wewe, lazima ushike agano langu, wewe na wazao wako baada yako na vizazi vijavyo. 10Hili ni agano langu na wewe pamoja na wazao wako baada yako, agano mtakalolishika: Kila mwanaume miongoni mwenu atatahiriwa. 11Mtatahiriwa, na hii itakuwa ni alama ya agano kati yangu na ninyi. 12Kwa vizazi vijavyo, kila mwanaume miongoni mwenu mwenye siku nane ni lazima atahiriwe, pamoja na watakaozaliwa nyumbani mwako au walionunuliwa kwa fedha kutoka kwa mgeni, wale ambao sio wa uzao wako. 13Awe amezaliwa nyumbani mwako au amenunuliwa kwa fedha yako, ni lazima atahiriwe. Agano langu katika mwili wako litakuwa ni agano la milele. 14Kila mwanaume asiyetahiriwa, ambaye hajapata tohara ya mwilini, atatengwa na watu wake; amelivunja agano langu.”
15Pia Mungu akamwambia Ibrahimu, “Kwa upande wa Sarai mkeo, hutamwita tena Sarai, bali jina lake litakuwa Sara. 16Nitambariki, na hakika nitakupatia mwana kwake. Nitambariki ili awe mama wa mataifa; wafalme wa mataifa watatoka kwake.”
17Ibrahimu akaanguka kifudifudi, akacheka na kusema moyoni mwake, “Je, mtu wa miaka mia moja aweza kuzaa mwana? Je, Sara atazaa mtoto katika umri wa miaka tisini?” 18Ibrahimu akamwambia Mungu, “Laiti Ishmaeli naye angeshiriki baraka yako!”
19Ndipo Mungu akasema, “Ndiyo, lakini mkeo Sara atakuzalia wewe mwana, nawe utamwita jina lake Isaka.#17:19 maana yake Anacheka Nitalithibitisha agano langu naye kama agano la milele kwa ajili yake na wazao wake baada yake. 20Kuhusu Ishmaeli, nimekusikia. Hakika nitambariki; nitamfanya awe na uzao mwingi na nitaongeza sana idadi yake. Atakuwa baba wa watawala kumi na wawili, nami nitamfanya awe taifa kubwa. 21Lakini agano langu nitalithibitisha kwa Isaka, ambaye Sara atakuzalia mwaka ujao majira kama haya.” 22Alipomaliza kuzungumza na Ibrahimu, Mungu akaondoka kwa Ibrahimu.
23Siku hiyo hiyo, Ibrahimu akamchukua Ishmaeli mwanawe na wote waliozaliwa nyumbani mwake, pamoja na wale walionunuliwa kwa fedha zake; kila mwanaume wa nyumbani mwake akawatahiri, kama Mungu alivyomwagiza. 24Ibrahimu alikuwa na umri wa miaka tisini na tisa alipotahiriwa; 25naye Ishmaeli mwanawe alitahiriwa akiwa na umri wa miaka kumi na tatu. 26Ibrahimu na Ishmaeli mwanawe walitahiriwa siku hiyo hiyo. 27Wanaume wote nyumbani mwa Ibrahimu, waliozaliwa nyumbani mwake na walionunuliwa kwa fedha kutoka kwa wageni, walitahiriwa pamoja naye.
اکنون انتخاب شده:
Mwanzo 17: NENO
هایلایت
به اشتراک گذاشتن
کپی
می خواهید نکات برجسته خود را در همه دستگاه های خود ذخیره کنید؟ برای ورودثبت نام کنید یا اگر ثبت نام کرده اید وارد شوید
Neno: Maandiko Matakatifu™ NMM™
Hakimiliki © 2018, 2024 na Biblica, Inc.
Imetumiwa kwa ruhusa.
Haki zote zimehifadhiwa duniani kote.
Kiswahili Contemporary Scriptures™
Copyright © 2018, 2024 by Biblica, Inc.
Used with permission. All rights reserved worldwide.