YouVersion Logo
Search Icon

Zaburi 139:1-18

Zaburi 139:1-18 BHN

Ee Mwenyezi-Mungu, wewe umenichunguza; wewe wanijua mpaka ndani. Nikiketi au nikisimama, wewe wajua; wajua kutoka mbali kila kitu ninachofikiria. Watambua nikienda au nikipumzika; wewe wazijua shughuli zangu zote. Kabla sijasema neno lolote, wewe, ee Mwenyezi-Mungu, walijua kabisa. Uko kila upande wangu, mbele na nyuma; waniwekea mkono wako kunilinda. Maarifa yako yapita akili yangu; ni makuu mno, siwezi kuyaelewa. Nikimbilie wapi ambako roho yako haiko? Niende wapi ambako wewe huko? Nikipanda juu mbinguni, wewe upo; nikijilaza chini kuzimu, wewe upo. Nikiruka hadi mawio ya jua, au hata mipakani mwa bahari, hata huko upo kuniongoza; mkono wako wa kulia utanitegemeza. Kama ningeliomba giza linifunike, giza linizunguke badala ya mwanga, kwako giza si giza hata kidogo, na usiku wangaa kama mchana; kwako giza na mwanga ni mamoja. Wewe umeniumba, mwili wangu wote; ulinitengeneza tumboni mwa mama yangu. Nakusifu maana nimefanywa kwa namna ya ajabu, matendo yako ni ya ajabu; wewe wanijua kabisakabisa. Umbo langu halikufichika kwako nilipotungwa kwa siri na ustadi ndani ya dunia. Wewe uliniona hata kabla sijazaliwa, uliandika kila kitu kitabuni mwako; siku zangu zote ulizipanga, hata kabla ya kuweko ile ya kwanza. Ee Mungu, mawazo yako ni makuu mno; hayawezi kabisa kuhesabika. Ningeyahesabu yangekuwa mengi kuliko mchanga. Niamkapo, bado nipo pamoja nawe.